12/14/06

SUALA HILI LINATUFUNDISHA NINI?



Katika pitapita yangu katika nchi hizi za Ulaya ya Magharibi mara nyingi nimekuwa nikikutana na changamoto za namna mbalimbali pamoja na vioja kadhaa. Lakini suala kubwa sana ambalo limenishtua sana na kunikera kiasi fulani ni kukuta wanyama wa aina mbali mbali katika hifadhi maalum “zoo” jijini Copenhagen nchini Denmark ambao aghalabu hupatikana katika uwanda wa kitropiki pamoja na Ikweta. Matarajio yangu mimi yalikuwa ni kwenda pale katika hifadhi kuangalia wanyama ambao wanapatikana katika nchi za baridi kama dubu, “moose, seals, llama, walrus” na kadhalika ambao sikupata kuwaona wakati natembelea mbuga zetu kwa kuwa hawapatikani kwetu katika nchi za joto. Wanyama hawa ambao niliwakuta katika hifadhi ya jiji tajwa hapo juu ni kama vile swala wa aina mbali mbali, vifaru, twiga, nyumbu, kangaroo, simba, nyani, ngedere, sokwe na ndege wa aina mbalimbali kama vile korongo, heroe batamaji na kadhalika. Wanyama hao pichani, pamoja na wengine ambao sijachapisha picha zao hapo niliwakuta katika hifadhi tajwa. Sasa sijajua kama wanyama hawa wapo hapa kihalali ama wamebebwa kwa njia ambazo wao wenyewe wanazijua Kwa hiyo basi kwa miaka michache sana ijayo halitakuwa suala la ajabu sana kukuta sisi ambao tunatoka katika uwanda wa kitropiki tunakwendaUlaya na kutazama wanyama ambao kwa asili walikuwa kwetu, ila kutokana na sababu ambazo mimi binafsi sijazifahamu wamehamia katika nchi za baridi. Kusema kweli hiki ni kioja ingawa najua kuna baadhi ya watu hawaoni athari za suala hili kwa uchumi kama wa nchi zetu changa ambazo bado tunahitaji pesa za watalii kwa kiasi kikubwa. Naomba utazame picha hizo (ambazo nilizipiga Ulaya, sio Serengeti) na utoe mtazamo wako, kwamba iwapo simba, twiga, nyumbu, nyati na wanyama wengine wa Afrika na Asia wanapatika nchi za baridi za Ulaya, kuna haja gani ya watalii kwenda Afrika, Amerika ya Kusini na Asia kutazama wanyama hawa wakati wanapatikana kwao?
Jadili!