31/07/2007

SAFU ZA MILIMA YA USAMBARA

UTANGULIZI

Safu za milima ya Usambara ni sehemu tu ya safu za milima ya tao ya mashariki "eastern arc Mountains". Milima hii inaunganishwa na safu ya milima ya Udzungwa na Uluguru katika uhifadhi. Inasifika kwa kuwa na viumbe wengi wa namna ya pekee (endemic), kwa hiyo inapewa umuhimu mkubwa sana katika utunzaji wake na taasisi za kimataifa kama vile 'Critical Ecosystem Partneship Fund (CEPF), International Centre for Insect Physiology and Ecology (ICIPE) pamoja na 'Birdlife International'. Safu za milima hii zinaambaa ambaa toka Muheza, Korogwe hadi Lushoto katika mkoa wa Tanga.Picha: Sehemu ya Msitu wa Kandelekampaa katika milima ya Usambara iliyoathiriwa kwa moto na kilimo, katika Kijiji cha Ndabwaa kata ya Malindi wilaya ya Lushoto


UMUHIMU WAKE
Safu za milima hii ni chanzo cha mito mingi sana, kama vile mto Zigi, mto Pangani na mto Umba, lakini sehemu kubwa ya misitu ya safu hizi imeharibiwa sana, hasa maeneo ya Lushoto na Korogwe, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu ambao kwa kiasi kikubwa hutegemea shughuli za kilimo na upasuaji wa mbao. Maeneo yaliyoathiriwa sana na shughuli hizi ni yale ya Usambara Magharibi, hasa wilayani Lushoto. Huku ndio sehemu kubwa sana ya misitu hii imefyekwa ama kuchomwa moto kabisa, hasa katika vijiji vya Ndabwa, Magamba na Lukozi. Kwa upande wa wilaya ya Muheza, angalau kuna matumaini, kwani misitu ya upande huu imetunzwa kwa kiasi cha kuridhisha. Ikumbukwe kuwa matunda na mboga mboga kutoka wilaya hizi hutoka katika mashamba ambayo ama yapo pembezoni mwa misitu hii ama yanapata maji yake toka katika misitu hii.Picha Juu: Mto mkuzu, ambao hutoka katika milima ya Usambara. Mto huu ni tegemeo sana kwa wakazi wa vijiji vingi vya Lushoto kwa umwagiliaji na matumizi ya nyumbani.

Pichani: Kabichi ambazo hulimwa katika mashamba yaliyo katika safu za Milima ya Usambara

ELIMU YA MAZINGIRA
Kuna taasisi kadhaa ambazo zinajihusisha na kuelimisha jamii zilizo katika maeneo haya juu ya kutunza safu za milima hii, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha utalii rafiki wa mazingira (eco-tourism). Taasisi hizi ni kama vile Friends of Usambara Society (FOU), West Usambara Women Education (WUWE), Lushoto Youth Development Network na kadhalika. Hata hivyo bado juhudi zaidi zinahitajika katika kupunguza athari hizi.

13/06/2007

NAFASI ZA UONGOZI KATIKA JUMUIYA YA WANABLOGU WA TANZANIA

OMBA NAFASI ZA UONGOZI
Ndugu msomaji wa blogu hii, kuna nafasi mbali mbali za uongozi zimetangazwa katika Jumuiya ya Wanablogu wa Watanzania. Unaruhusiwa kugombea nafasi yoyote, na si lazime uwe na blogu ili kupata nafasi hizo. Nafasi hizo zinazonadiwa ni za Mwenyekiti, Mhazini, Katibu na nyinginezo.

MAMBO YA KUZINGATIA
Tuma picha yako ukiambatanisha na wasifu wako, pamoja na sababu zinazokutuma kugombea na nafasi unayogombea. Ueleze ni kitu gani unataka kuifanyia Jumuiya katika kuikuza. Tuma maelezo yako kwa 'mijasayi@yahoo.com'.
Kwa maelezo zaidi tafadhali tembelea blogu ya Jumuiya 'http://blogutanzania.blogspot.com'

22/05/2007

MWAKA MMOJA WA KUJADILI WATIMIA!

TOVUTI YATIMIZA MWAKA
Leo tarehe 22/05/2007 tovuti hii inatimiza mwaka mmoja tangu izinduliwe rasmi mwaka jana 2006. Tarehe kama hii mwaka jana ndipo makala ya kwanza ilibandikwa mahali hapa. Nakumbuka jinsi ilivyokuwa vigumu kuamua cha kuandika, lakini hatimaye mambo yakaenda vyema na mpaka leo naendelea kusimama.
Tangu izinduliwe rasmi mwaka jana, tuvuti hii imefanyiwa madiliko ya mwonekano mara tatu na bado itaendelea kuboreshwa kwa kuongeza mambo mapya ambayo kwa sasa yanaandaliwa.
Kimsingi mawazo ya kuanzisha blogu hii yalitokana na ushawishi mkubwa wa Mzee wa "Baragumu", ambaye ni swahiba wangu wa siku nyingi sana, tangu tukiwa tunasoma shule moja ya sekondari mkoani Iringa. Huyu ndiye aliyenishawishi kwa kiasi kikubwa kuanzisha tovuti hii na baadaye akafuatiwa na mwanablogu nguli, Mzee wa "Jikomboe". Pamoja na hawa pia kuna kundi kubwa sana la wanablogu wenzangu ambao naweza kuujaza ukurasa huu kama nitaamua kuwataja mmoja baada ya mwingine ambao wamekuwa wakitoa michango yao mbali mbali ya mawazo katika kuiboresha tovuti hii, hawa nao nawapa shukrani za pekee.
Nayathamini sana mawazo yenu na naomba tuendelee kushirikiana ili tuweze kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kuboresha mazingira yetu.
Naahidi kuendelea kuweka makala za kuzua mijadala ya kuboresha maisha yetu mahali hapa, na naomba tuendelee 'kujadili' kama kawaida yetu.

30/04/2007

SAFISHA HAPA.....CHAFUA PALE!

UTANGULIZI

Ni suala la kawaida kukuta barafu/theluji katika miinuko ya maeneo mbali mbali ya nchi zilizo katika Tropiki ya Kansa, yaani nyuzi 23.26' kaskazini mwa Ikweta, hasa wakati wa majira ya baridi. Barafu/theluji huongezeka zaidi kama unazidi kuelekea kaskazini katika mzingo wa Aktiki (nyuzi 66.33'). Kwa wenyeji wa maeneo haya, huu ni msimu wa michezo ya wakati wa baridi kama vile kuteleza katika theluji na kutembea katika maji yaliyoganda (barafu). Lakini kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri kama baiskeli, magari, treni na ndege ni msimu usiopendeza sana. Kwa upande wa baiskeli, magari na ndege, ni msimu wa kubadilisha magurudumu. Magurudumu yanayotumika wakati wa kiangazi ni tofauti na yale yatumikayo wakati wa baridi. Tofauti yake ni kwamba magurudumu ya msimu wa baridi huwa na misumari midogo midogo katika uso wake, ili kuleta msuguano wa kutosha (friction) wakati chombo kinapopita katika barafu ama theluji. Bila magurudumu ya namna hii ni rahisi sana kwenda nje ya barabara kama kuna theluji, kwa sababu huwa inateleza sana. Theluji pia hujaa katika reli na kusababisha utelezi. Ni kawaida kwa maeneo haya kukuta vyombo vya kusafisha theluji barabarani kila asubuhi.

UONDOAJI WA THELUJI
Theluji ikishafagiliwa, hukusanywa mahali na kisha kuzolewa katika magari makubwa na kwenda kutupwa. Shida yake huanzia hapa, kwamba mara nyingi katika nchi hizi theluji hutupwa katika bahari ama maeneo mengine ambayo ni oevu. Iwapo kunakuwa na joto theluji hii huyeyuka na kuwa maji. Wanamazingira hawapendezwi na suala hili la kutupa theluji na barafu katika maeneo haya. Madai yao ni kuwa, mara nyingi theluji inayokusanywa mitaani huwa na takataka sana, kwa hiyo unapoikusanya na kwenda kuimwaga baharini ama maeneo mengine unakuwa unasababisha uchafu mahali hapo. Ieleweke pia kuwa theluji hii huweza kuambatana na mafuta yanayotumika kulainishia ama kuendeshea mitambo, hivyo kama itatupwa katika maeno yenye unyevu basi itasababisha kufa kwa viumbe hai ambao hutegemea maji hayo kwa maisha yao kama vile samaki na vyura. Hali kadhalika mafuta huganda katika mbawa za ndege wavuvi, hivyo hushidwa kuruka kujitafutia riziki zao na hivyo hufa kwa njaa.

SULUHISHO
Kutokana na malalamiko ya wanamazingira kuhusiana na uchafuzi huu, wazoaji wa theluji (hasa halmashauri za miji) wameamua kutupa theluji hii katika maeneo maalum yalitengwa kwa ajili hiyo (dump sites). Kwa hiyo maeneo hayo huwa ni maalum kwa ajili ya kumwaga theluji na barafu na uchafu unaoambatana navyo. Bado wanamazingira hawajaridhika na kitendo hiki, kwa sababu wanasema unatibu tatizo moja huku ukisababisha jingine la uchafuzi wa mazingira. imsingi barafu na theluji ni maji, na wanaomwaga wanajua kuwa wakati wa kiangazi huwa inayeyuka, suala linalogombaniwa hapa ni taka zinazoambatana na theluji ama barafu, kuwa ndizo zinazoleta madhara katika mazingira. Mpaka sasa bado kuna mgongano wa mawazo kuhusu nini kifanyike ili kutatua mvutano huu, tusubiri tuone matokeo yake.
Kwa upande wa nchi za Kitropiki hakuna tatizo la barafu, katika miji, ila suala la utupaji ovyo wa taka lipo na limeshamiri sana.

Barafu iliyokusanywa, ikisubiri kuzolewa na kwenda kutupwa!

12/04/2007

FAHAMU MVUA ZA TINDIKALI

MVUA ZA TINDIKALI

UTANGULIZI

Katika makala zangu zilizopita, niliwahi kudokeza kidogo kuhusu mvua za tindikali, ama kwa Kiingereza ’Acid rains’. Leo nafafanua zaidi kuhusu mvua hizi, nikianzia na chanzo, madhara yake, namna ya kupima madhara yake na namna ya kupunguza mvua hizi.

CHANZO CHA MVUA ZA TINDIKALI
Kimsingi, mvua za tindikali husababishwa na chembe chembe nyevunyevu na zile kavu za baadhi ya gesi ambazo kwa pamoja huwa zinaelea angani. Chembe chembe hizi aghalabu ni tindikali ya salfuriki ama naitriki. Kuna vyanzo vikuu viwili vya tindikali hizi katika anga. Kwanza ni vyanzo vya asili ambavyo mwanadamu hana mamlaka navyo na hana namna ya kuvizuia, kama vile volkano na kuoza kwa mimea. Baadhi ya mimea inapooza huzalisha kiasi fulani cha tindikali, ambayo iwapo itakutana na maji basi huwa na madhara katika ardhi. Vivyo hivyo, kunapotokea mlipuko wa volkano, majivu pamoja na gesi kutoka katika volkano hizi huwa na chembe chembe za tindikali ambazo hupelekwa angani na kuelea. Kwa hiyo vitu hivi vikichanganyikana na maji au unyevu katika anga hufanya tindikali ambazo nimezitaja hapo juu.
Pili, viwanda vingi hasa vinavyozalisha nishati kwa kutumia tungamotaka hasa makaa ya mawe, mkaa na kuni huzalisha hewa nyingi sana za oksaidi za salfa na naitrojeni (SO2) na (NOx). Sasa basi, iwapo hewa hizi zitachangayikana na unyevu ulio angani pamoja na kemikali nyingine zinazoelea angani basi tindikali tajwa hapo juu na nyingine nyingi hutokea. Kuna wakati gesi hizi huweza kusafirishwa mbali zaidi kwa njia ya upepo na kuleta madhara mahali mbali kabisa na chanzo chake.

2H2O + 2SO2 + O2 → 2H2SO4 (dhaifu)
Hii ni tindikali ya salfuriki.

Mchanganyiko wa tindikali ya naitriki huwa kama ifuatavyo:
NO2 + OH· → HNO3 (dhaifu)

CHEMBE CHEMBE NYEVU
Kama nilivyodokeza katika aya za hapo juu, chembe chembe za hizi tindikali huweza kuwa nyevu ama kavu. Kwa upande wa chembe chembe nyevu, hizi huwa katika mfumo wa mvua, manyunyu, ukungu ama theluji. Sasa basi, iwapo upepo utapeperusha chembe chembe hizi mahali ambapo hali ya hewa ni ya unyevu, basi chembe chembe hizi hutua katika uso wa dunia kama mvua, ukungu, manyunyu ama theluji kulingana na hali ya hewa ya mahali husika. Sasa basi maji ya mvua ama ukungu ama manyunyu yaliyo na tindikali huwa na madhara kwa viumbe hai ambao wanatumia maji haya kwa namna moja ama nyingine. Makali ya athari ya tindikali hii hutegemena na kiasi cha tindikali kilicho katika maji haya, aina za udongo, wanyama na mimea inayotegema maji haya.

CHEMBE CHEMBE KAVU
Katika maeneo ambayo hali ya hewa ni kavu kabisa, kama ilivyo katika jangwa, chembe chembe za tindikali huweza kuchanganyika na vumbi ama moshi na kutua katika ardhi vikiwa katika hali ua ukavu hivyo hivyo. Vumbi ama moshi wenye tindikali hii huganda katika vitu mbali mbali kama vile mapaa ya nyumba, magari, madaraja, majengo na mimea. Sasa iwapo mvua kidogo tu itanyesha na kusafisha vitu hivi basi tindikali hii husambaa na kuleta madhara katika maeneo mbali mbali.

ATHARI ZA MVUA ZA TINDIKALI
Mvua za tindikali huchangia sana kuongeza sumu katika maeneo mbali mbali kama vile mito, maziwa na wakati mwingine husababisha mimea kupukutika ama kufa kabisa, kwa sababu tindikali hii huunguza majani na mashina ya mimea hii. Mvua hizi husababisha kuoza kwa mapaa yanayoezekwa kwa bati ama chuma na pia huathiri sana rangi za majengo. Gesi za oksaidi za salfa na naitrojeni pia huathiri uwezo wa kuona pamoja na kupumua kwa mwanadamu.

Athari Katika sehemu oevu
Sehemu oevu ni zile ambazo zina unyevu nyevu katika msimu wote wa mwaka kama vile mito, maziwa, madimbwi na ardhi oevu. Katika maeneo haya, mvua za tindikali huathiri wanyama na mimea ambavyo hutegema maji haya. Kwa kuwa maji haya yanakuwa na kiasi kikubwa cha tindikali kuliko uwezo wa viumbe hawa kuhimili, basi viumbe hawa hushidwa kuishi na hivyo hufa. Majani ya mimea katika maeneo haya hupukutika, kwa sababu tindikali hizi huunguza mimea hii na hivyo kuifanya kushindwa kusanisi chakula (photosynthesis).

Athari Katika Misitu
Kimsingi, jamii mbali mbali za mimea hutofautiana katika ustahimilivu wa madhara ya kimazingira. Mimea hutofautiana katika ustahimilivu wa ukame, baridi, joto kali, maji mengi (mafuriko), ukosefu wa mwanga na uharibifu mwingine. Hivyo basi, katika misitu ya namna mbali mbali, athari za tindikali hutofautiana. Ila athari za jumla za tindikali katika misitu ni kuchelewa kukua kwa mimea, kupukutika majani na kufa kabisa kwa mimea. Marekani, hasa katika misitu yake ya upande wa mashariki imeathirika sana na madhara haya ya kukauka kwa mimea, hasa maeneo yaliyo karibu na milima ya Appalachian. Hali kadhalika nchi kama Kanada, Urusi na nyingine za Ulaya ya Mashariki zimeathirika sana kutokana na mvua hizi za tindikali.

Athari Katika Rangi za Majengo, Magari na Metali
Rangi hutengenezwa kutokana na mchanganyiko wa kemikali mbali mbali. Hivyo basi, iwapo mvua za tindikali zitatua katika maeneo yaliyopakwa rangi huweza kubabua rangi hizi na kusababisha kitu kilichopakwa rangi kupoteza hadhi yake. Mfano, kama rangi ya gari itapukutika kutokana na tindikali hizi bila kupakwa tena, basi kutu itavamia na kuozesha gari husika. Hali kadhalika, metali za namna mbali mbali hupakwa ramgi ili kuchelewesha kutu, hivyo kama tindikali itaondoa rangi hizi basi kutu uweza kuathiri metali hizi. Mfano wa metali hizi ni katika madaraja, nguzo za chuma, sanamu za vyuma na mihimili mbalimbali. Athari hizi huenda kwa namna hii hii katika majengo mbalimbali yaliyopakwa rangi.

Athari za Uoni (visibility) kwa Mwandamu
Hapo juu nilidokeza kuwa gesi za oksaidi za salfa na naitrojeni husababisha madhara katika uwezo wa kutazama wa mwanadamu. Kunapokuwa na msongamano wa hewa hizi katika anga, mwanadamu hawezi kutazama mbali kwa sababu hewa hizi hufanya ukungu ambao huzuia kuona mbali. Athari za namna hii ni maarufu sana nchini China, hasa katika maeneo ambayo hutumia makaa ya mawe kuzalisha nishati kama vile katika jiji la Shanghai katika Jamhuri ya watu wa China.

Madhara mengine
Madhara mengine kwa mwanadamu ni kuwa, iwapo atavuta hewa hizi zinazosababisha mvua za tindikali katika mfumo wake wa hewa, basi huweza kuathiri uwezo wa mapafu kufanya kazi, hivyo huweza kuata magonjwa kama pumu na kansa.


UPIMAJI WA MVUA ZA TINDIKALI
Utambuzi wa mvua za tindikali hupimwa kwa kutumia skeli ya ‘pH’. Kipimo hiki pia hutumika kupima kiwango cha alkali ama besi katika ardhi na maji. Maji yaliyotakaswa (purified water) kwa kawaida huwa na kiwango cha 7.0 katika kipimo tajwa. Jinsi kipimo hiki kinavyofanya kazi ni kwamba, kuanzia katika kiwango cha 7 kushuka chini huashiria ongezeko la tindikali na kuanzia 7.5 hadi 14 huashiria ongezeko la alkali ama besi. Kwa hiyo kiwango cha 7 katika pH huchukuliwa kama ndio alama ya katikati kati ya alkali na tindikali.


NAMNA YA KUPUNGUZA MVUA ZA TINDIKALI
Kwa maneno rahisi mtu anaweza kufikiri kuwa namna rahisi ya kupunguza msongamano wa gesi zinazosababisha mvua za tindikali ni kupunguza moshi kutoka viwandani moja kwa moja. Hili si jambo rahisi sana namna hiyo kutokana na sababu mbalimbali. Nilieleza kuwa mojawapo wa vyanzo vya gesi hizo ni pamoja na nguvu za asili kama vile volkano na kuoza kwa mimea. Hakuna mwanadamu mwenye uwezo wa kuzuia volkano, sana sana ikitokea huwa tupewa maonyo ya kuiepuka kwa kukimbilia mahali salama. Hivyo basi, matukio kama haya yataendelea kusababisha mvua za tindikali. Hali kadhalika si rahisi sana kuzuia mimea isioze na kusababisha gesi hizi. Kuoza kwa mimea husaidia kuleta rutuba katika ardhi, kwa hiyo hili nalo hatuna mamlaka nalo sana. La muhimu hapa ni kupunguza matumizi ya makaa ya mawe, kwa kutumia vyanzo vingine safi vya nishati kama umeme wa jua na umeme wa nguvu ya maji. Suala hili lmekuwa gumu kutekelezeka kutokana na mgongano wa sera katika nchi mbali mbali. Lakini hata hivyo kuna matumaini katika kufanikiwa, kwa sababu sasa dunia imeamka na kuanza kuhangaikia kupunguza hewa zenye sumu katika anga. Mojawapo ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kutengeneza magari na mitambo mingine inayotumia mafuta yaliyochanganywa na mafuta ya mimea, (biodiesel).
Hali kadhalika, kumeanzishwa sheria kuwa, anayechafua zaidi anga kwa moshi wenye sumu na alipe zaidi kadri ya anavyochafua. Angalau sheria hizi zinafanya wachafuzi washituke kidogo na kuona kuwa wanahusika na uchafuzi huu.

Unaweza kusoma zaidi kuhusu mvua za tindikali hapa, hapa ama hapa.